MWAJOMBENEWS


Hii ni blog mpya inayo milikiwa na EVANS SOMBE; inayokuletea habari mpya na za uhakika punde tu zinapotokea pia waweza kupakua nyimbo na video bure kabisa.Endelea kuwa mjanja kwa kutembelea blog yetu kwa habari motomoto.


Breaking

Thursday, July 13, 2017

FAHAMU MADHARA YA MITANDAO YA KIJAMII




Mitandao ya kijamii ni njia za kielektroniki ambazo hutumiwa na watu kupitia makundi makubwa kwa madogo kufikisha mawasiliano. Kwa njia hiyo, watu hushirikishana, uwazi hutamalaki, mazungumzo huwa bayana na pia hali ya kuunganishana hudhihirika. Baadhi ya mitandao kijamii ni pamoja ni: Facebook, Instagram, Tweeter, Jamii Forum, Whatsap, Wikipedia, Youtube, Blog, Email, Flickr, MySpace, LinkedIn na Podcast, kuitaja japo kwa uchache tu.
Ninaendelea kuamini kuwa wakati mitandao hiyo ya kijamii inaibuka miaka ya 2000, hakukuwa na Lengo baya dhidi ya Matumizi yake. Facebook ilianza mnamo miaka ya 2001 wakati huo Mark Zuckerberg na wanafunzi wenzake wa Havard University walipogundua mtandao huo. Hadi kufikia mwaka 2013, Facebook imekuwa na watumiaji wapatao bilioni 1.1. Tweeter, pia , ni mtandao wa hivi majuzi (mwaka 2006), lakini leo hii una watumiaji wengi sana.


Kwa takwimu chache nilizonazo, mitandao ya kijamii iliyoanzia ughaibuni, inatumika sana Nigeria (72%) na Marekani (48%). Kwa Tanzania, takribani 15% ya watanzania hutumia mitandao ya kijamii. Fikiria kama 62% ya watanzania wana simu, je unadhani [kwa wale wenye smartphone] hawawezi kujiunga katika mitandao ya kijamii mbalimbali? Zaidi ya yote, kwa mwaka 2012, watanzania wapatao 682,000 walikuwa wamejiunga na Facebook. Baada ya miezi sita kupita [katika mwaka huo huo], ongezeko hilo lilipanda kwa zaidi ya watu 56,580. Hii ina maana kuwa miaka mitano baadaye [mwaka huu 2017] watumiaji wanaweza kuwa 964,900.
Kama mitandao ya kijamii imekuwepo kwa malengo ya kuhabarishana juu ya masuala mbalimbali ya ajira, uchumi, utamaduni, uongozi na biashara; kujengana kimawazo; kupata burudani na kuelimishana; nini athari mbaya zinazojitokeza miongoni mwa watumiaji wa mitandao hiyo?
Yako madhara mengi yatokanayo na utumiaji mbaya wa mitandao ya kijamii. Yafuatayo ni baadhi tu ya madhara hayo:
Mosi, kusababisha watu kutapeliwa. Kupitia mitandao ya kijamii, kuna watu wasio waungwana wanaoitumia vibaya kiasi cha kuwatapeli wenzao. Mara kadhaa, kupitia vyombo vya habari; magazeti, redio na runinga, tumesikia watu wakitapeliwa kwa njia ya mitandao ya kijamii hususani Email.
Pili, baadhi ya mitandao ya kijamii imechukuliwa katika sehemu vituo vya kuhamasisha biashara za ngono. Si ajabu tena kuona baadhi ya wanawake wakijiuza kupitia Instagram, Facebook na Whatsap. Kwa bahati mbaya, baadhi ya watumiaji wa mitandao hii wameshindwa kutambua namna wanavyoshawishiwa kujiingiza katika biashara hizo.
Tatu, kuharibu mahusiano ya baadhi ya watu. Wapo wanajamii ambao kila kukicha wanaugulia maumivu baada ya wenzi wao kujiingiza kwenye mahusiano na watu wanaofahamiana nao pengine walisoma nao, walikuwa nao katika maeneo ya kazi na huenda pia walipotezana muda lakini waliwahi kuwa wapenzi. Hali hii imepelekea vilio kila kukicha kwenye baadhi ya familia. Chanzo cha huo uozo kikiwa ni mitandao ya kijamii.

Nne, kudhalilishana kupitia mitandao. Ni wazi kuwa mitandao inahusisha watu wengi kama nilivyojaribu kukubainishia takwimu japo kwa uchache. Wapo baadhi ya watu ambao ama hukosana na wenzao au hupenda tu kusasisha picha za wenzao kupitia mitandao ya kijamii. Huenda ni kweli kupitia picha zinazosasishwa, watendaji wa mambo hayo wametenda. Lakini cha kushangaza badala ya kuelekezana kwa namna nyingine, watumaji wa picha wamejikuta wakidhalilisha wenzao kupitia mitandao hiyo.
Tano, kupoteza muda wa kufanya masuala mengine. Kwa kuwa mitandao hii ya kijamii imeshika kasi sana, wapo baadhi ya watu wanojikuta wanatumia muda mwingi katika mitandao hii ya kijamii. Katika utafiti mmoja uliofanywa nchini Tanzania, unaonesha watumiaji wa mitandao ya kijamii hutumia kati ya dakika thelathini hadi masaa matatu kwa siku [huo ukiwa ni wastani wa muda kwa watumiaji wote]. Kumbuka, wapo wanaotumia zaidi ya masaa matano kwa siku. Swali: shughuli nyingine zinaendaje ikiwa mtumiaji ana muda mwingi kiasi hicho?
Sita, kuibua hisia kali na mbaya kwa baadhi ya watu. Chukulia mfano wa ajali ya tukio lile la Lucky Vincent. Watu wengi walituma na kusasisha picha za ajali ile. Unadhani watu wangapi wana mioyo ya kuvumilia? Je, umewahi kudhani kabla juu ya wale wenye mioyo myepesi zaidi na kupaniki kwa haraka? Baada ya tukio lile, wangapi katika familia za wafiwa wameendelea kukweweseka kutoka na tukio lenyewe? Nadhani, tufike mahala tuwe makini na namna ya kutumiana ujumbe, picha na kadhalika. Si vema sana kwa matukio ya kuogofya kuyasasisha kupitia mitandao ya kijamii. Ni kweli tunahabarishana lakini tuangalie namna. Watu wengine waliendelea kusasisha picha hata baada ya watoto wale kuzikwa. Hii ilikuwa na maana gani? Je, ni kuamsha upya hisia za wafiwa kila watizamapo picha hizo?
Saba, mitandao ya kijamii kwa namna nyingine imechangia watumiaji wake kuharibu lugha adhimu ya Kiswahili. Unaweza usilione hili kwa macho mawili lakini ukilitazama kwa jicho la tatu, watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii aina ya Facebook wanaharibu Matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili. Kumekuwa na vifupisho vingi, changanya msimbo [code mixing] kwa sana na kadhalika. Yote haya hayana maana kwa wajifunzaji lugha na wataalam wa lugha pia.

                                               
Nane, sehemu ya kuzushia mambo. Sifa na hadhi ya mitandao ya kijamii imeendelea kushuka kwa kuwa baadhi ya watumiaji wabaya wa mitandao hiyo wametumia vibaya fursa kwa kuzusha vitu visivyokuwepo. Matokeo ya uzushi huo ni kushawishi watumiaji wa mitandao kuamini kwa haraka vitu vinavyozushwa. Kwa mfano; mara kadhaa kupitia Facebook na Whatsap, tumeshuhudia watu maarufu kutoka ughaibuni na kwingineko wakizushiwa vifo na wabaya wao. Bila kutambua athari za uzushi, wazushi hao wamejipatia umaarufu.
Kwa jicho la kisaikolojia, madhara ya mitandao ya kijamii yako kwa namna hii:
Mosi, kusababisha baadhi ya watu kupoteza maisha yao. Kuna baadhi ya watu wanapogundua kuwa wamedhalilishwa huchukua huwaza sana na matokeo ya sonona ni pamoja na kuchukua hatua kama kujiua.
Pili, kujifunza mambo mabaya kama ngono. Kadri unavyoona kitu fulani ndivyo akili yako inavyoshawishika kulifanyia kazi katika utendaji. Chukulia mfano, kila kukicha wewe ni mtu wa kutazama video au clip za ngono kupitia Youtube, matokeo ya utazamaji huo yataathiriwa kiakili na hatimaye hisia zako zitapelekea kutenda kile ukionacho.
Tatu, kujitenga na watu. Unapotumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii, tambua ya kuwa unafika wakati hali ya kujitenga hutokea ili ufurahie ulimwengu wa teknolojia. Hali huathiri maendeleo ya familia, kazi na mahusiano miongoni mwa wanajimii kwa ujumla. Mtu anayechati sana hapendi kuwa karibu na watu wengine! Hebu thibitisha hii leo mahala ulipo kama ni kwenye daladala, nje ya darasa pamoja na nyumbani. Angalia jinsi mtu anavyohangaika kwenye simu peke yake.
Nne, kupungua uwezo wa kutafakari. Akili ya mwanadamu ipo kwa namna ya ajabu sana. Kuna muda, akili hutafakari yale yote yaliyoonwa, hisiwa, guswa, onjwa na kadhalika. Hata wakati umelala, michakato ya akili huendelea haisimami. Inapotokea unatumia sana mitandao ya kijamii, unapunguza uwezo wa kutafakari na hali hii pia inaathiri utendaji kazi wako. Angalia jinsi vijana wa shule wanatazama masuala yasiyoendana na vile wanavyosoma. Ripoti ya BBC News ya mwaka 2013 inasema asilimia 60 ya watumiaji wa Facebook, moja ya mitandao ya kijamii ni vijana na wanafunzi [wahanga wa mitandao ya kijamii]. Kwa wanafunzi wanaofanya vema katika mitihani kitaifa,  hujua namna njema kila wanapotumia mitandao ya kijamii kwa kuwa wanatambua fika mitandao hiyo inaathiri uwezo wao kiakili.
Mwisho, pale tunapoona madhara ya mitandao inatulazimu tufikiri vinginevyo. Kuna mambo makubwa matatu nayaita vigezogeu kitaalam variables. Panapo matumizi ya mitandao ya kijamii [kigezogeu kinachojitegemea] lazima pia pawe na mchakato [sheria mf: Sheria ya Makosa ya Mitandao na kadhalika, Vyombo vya Usalama, Elimu juu ya Matumizi Sahihi ya Mitandao ya Kijamii inayopaswa kutolewa na familia, wanajamii pamoja na serikali inayoruhusu mitandao itumike] mwisho ni kigezogeu-maudhui au kigezogeu tegemewa [yale yaonekanayo, yaandikwayo]. Kigezogeu cha tatu ni matokeo ya vigezogeu vilivyotangulia kwa namna ya kuwa; kigezogeu cha kwanza na cha pili vikishirikiana vema, madhara (athari) katika kigezogeu cha tatu yatapungua. Ikiwa masuala haya matatu yatafanyika kwa namna ya kuchangamana, Tanzania itakuwa moja kati ya nchi yenye watumiaji bora wa mitandao ya kijamii ulimwenguni

imeandaliwa
NA INJILILEO
www.injilileo.com

No comments:

Post a Comment