saikolojia, elimu ambayo katika ulimwengu wa sasa wengi wanaisikia lakini
ni wachache wanaotambua umuhimu wake, achilia mbali maana ya neno lenyewe.
Injinia wa kwanza aliyeipa nguvu elimu hii ni
mwanasaikolojia wa Kijerumani, Wilhelm Wundt ambaye alifungua maabara iliyokuwa
ikifanya utafiti na kutibu watu kwa kisaikolojia, zoezi ambalo lilileta matokeo
ya kushangaza ulimwenguni. Huo ulikuwa mwaka 1879.
Saikolojia ni mtoto wa neno la Kigiriki lijulikanalo kama
psyche au akili na roho jina ambalo baadaye lilikuzwa na kufahamika kama
Psychology, tafsiri ikiwa ni Elimu ya Nafsi na Ufahamu.
Katika nchi zilizoendelea, somo hili linapewa nafasi ya juu
katika maisha ya binadamu kutokana na umuhimu wake. Wanasema wataalamu kuwa,
kuishi bila kujua tabia za vitu na watu, ukuaji wake na kujifunza mabadiliko
yake ni sawa na kutembea katika kamba ndogo ya maisha salama.
Saikolojia ni somo ambalo kila kukicha binadamu anatakiwa
kufundishwa kwa vile hakuna anachoweza kukifanya kisiguse akili na nafsi yake.
Inashauriwa kwamba ni lazima mtu ajifahamu mwenyewe, awafahamu wengine,
mazingira anayoishi na mabadiliko yake.
Maswali ya msingi yenye kumuongoza binadamu vizuri katika
maisha yake ni haya; Mimi ni nani, kwa nini niko hivi? Wale ni 80 akina nani,
kwa nini wako vile na tunapaswa kuwa vipi baadaye, pamoja na kujiuliza kwa nini
vitu vipo kama vilivyo.
Imebainika kwamba, mvutano wa nguvu za dunia na za binadamu
huongezeka mara dufu kwa mtu ambaye hajui Saikolojia ya Maisha. Dunia kama
sayari na mwanadamu kama kiumbe kila mmoja amekuwa
akitengeneza nguvu zake za kumuwezesha kuwepo, huku
uzalishaji wa nguvu hizo kwa upande mmoja ukikinzana vikali na mwingine, hata
hivyo madhara makubwa yamekuwa yakiwakuta binadamu ambao ndani yao kuna uhai.
Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kwamba, ufahamu wa nafsi na
akili umebaki kuwa kinga muhimu ya mwanadamu katika ulimwengu huu ambao umekuwa
ukibadilika mara kwa mara.
Hatari inayokuwepo kwa baadhi ya binadamu siku hizi hasa wa
ulimwengu wa tatu, ni ukosefu wa elimu hii muhimu, jambo ambalo limewafanya
watu wenyewe kwa wenyewe kuzalishiana nguvu za kuangamizana na kuiacha dunia
ikishinda.
Inahuzunisha pia kufahamu kwamba, mbali na binadamu
kushindana na mabadiliko ya ulimwengu na nguvu zake, wengi wao wamekuwa
wakipambana na nguvu zao wenyewe ndani ya miili yao bila kujijua, kiasi cha
kupoteza maisha.
Tafiti za wanasaikolojia zinaonesha kwamba, asilimia kubwa
ya matatizo yanayomwangaisha binadamu yanatokana na yeye mwenyewe au jamaa
zake, huku ushahidi ukionesha kuwa hata magonjwa ya kutisha
kama ya moyo, kansa, kisukari, vidonda ya tumbo na mengineyo
yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mawazo ya watu wenyewe.
WENGI kati ya watu wanaosumbuliwa na matatizo yanaoitwaya
dunia ni wale wanaopambana na nguvu zao bila kujua. Kwa kutumia akili zao
vibaya, hujitesa kwa kufikiri na kutafsiri vibaya matukio ya kila siku yanayotokea
duniani.
Kama nilivyowahi kusema katika moja ya makala zangu
nilizochapisha kwenye toleo la kitabu changu cha pili cha saikolojia ni kwamba
hakuna kitu kibaya katika ulimwengu kwa asili, isipokuwa mawazo ya mtu
mwenyewe.
Kwa mfano, tukizungumzia kufa ambapo watu wengi wanaamini
kwamba ni jambo baya, kuna wengine wanaona ni zuri ndiyo maana wapo wanaojiua,
na kama tukisema vita ni hatari, bado kuna watu wanafurahia
vita kwa vile si wote wanaowahurumia wafao vitani hata kama
wataona maiti zao barabarani kwa wingi.
Kama nilivyosema, duniani kuna nguvu mbili, ambazo ni za
watu wenyewe na za ulimwengu, hii ina maana
kuwa hata mawazo ya mwanadamu ni nguvu na mtu anaposumbukia
kuwaza jambo fulani kwa undani kiasi cha kuumiza moyo wake anakuwa anashindana
na nguvu zake mwenyewe.
Ifahamike kuwa kadiri mwanadamu anavyozidi kuongeza nguvu ya
kufikiri, iwe kwa kukua kimwili, kusoma na kujifunza mambo mengi zaidi, kwa
asili anakuwa anaongeza nguvu ambazo asipokuwa makini anaweza kufa akishindana
nazo badala ya kuzitumia katika kumsaidia kimaisha.
Kwa mfano, watu kutoka kabila la Wabarabeigi wanaopatikana
mkoani Manyara, nchini Tanzania wanaishi maisha ya kuwinda wanyama na kula
mizizi ya porini, hawawezi kukaa wakifikiri jinsi ya kupata gari kwa kuwa kwao
gari halina maana. Kwao maendeleo ni kuwinda na kuzaliana.
Kwa maana hiyo linapokuja suala la maisha magumu litatokana
na ukame na wala si ukosefu wa mitaji au kazi. Hawa hawawazi magari kwa sababu
hawajajifunza umuhimu wake, hawajui umuhimu wa kuwa na
zahanati, hospitali na wala bei ya mafuta haiwasumbui.
Lakini kwa Wachaga waliozoea umeme wakikosa huduma hiyo kwao hilo litakuwa ni
tatizo kubwa litakalowakosesha usingizi.
Vivyo hivyo, kwa watu waliozoea kutibiwa kwa sindano na
vidonge, wakikosa tiba hizo itakuwa rahisi kwao kufa, kwa sababu akili zao
zinatafsiri ukosefu huo kama tatizo kubwa kwao, lakini haiwi hivyo kwa
Wasukuma wanaoishi maporini kusikokuwa na hospitali za rufaa
wala umeme.
Tafsiri ya hili ni nini? Ni fikra zitokanazo na kujua mambo
na namna ya kuyawaza. Watu wengi siku hizi
wanajua utajiri, wanafahamu nini maana ya afya, wanaelewa
umuhimu wa maendeleo lakini siyo wote wenye uwezo wa kukutana na changamoto
hizo na kupata matokeo sahihi ya kile wanachokifahamu.
Kwenda hospitali kupimwa na kuambiwa kuwa una Kansa, Ukimwi,
Kisukari, Pumu, TB na magonjwa kama hayo, siyo jambo linalowasaidia wengi kwa
vile hawajui hatua ya kuelekea kwenye ujuzi huo wa mambo. Hapa ndipo elimu ya
saikolojia inapohitajika ili iweze kumsaidia mtu anayejua mambo hayo namna ya
kuyakabili, kuyaendeleza na kupata mafanikio.
Jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi wanaofahamu mambo
hawafaidiki nayo na pale wanapojaribu kutumia ujuzi wao walioupata shuleni,
wanajikuta wanaingia kwenye mapambano ya nguvu ya vile wanavyovifahamu.
Watu wengi leo hawalali usiku kucha wakipambana na yale
waliyoyafahamu, utakuta mtu kakonda kwa sababu katambua mpenzi wake si
mwaminifu, anakesha akilia bila kujua afanye nini kumaliza tatizo.
Mtu mwingine anakonda kwa sababu ni maskini, hana mtaji na
ajabu nyingine kuna wanaosumbukia hata kasoro za maumbile yao ambazo wameumbwa
nazo!
No comments:
Post a Comment